MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetangaza kuanza kutumika rasmi kwa punguzo la bei za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine kuanzia Machi Mosi mwaka huu.
Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Profesa John Nkoma, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, bei hiyo itakuwa ni sh 34.92 kwa dakika badala ya sh 115 iliyokuwepo hapo awali.
ProfNkoma alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupitiwa kwa taratibu zote ikiwemo kuyashirikisha makampuni ya simu na wadau wengine katika kupata maoni yao.
Alisema kutokana na kupitishwa kwa sheria hiyo, makampuni yote ya simu yatatakiwa kusaini mkataba kabla ya Machi 31 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ProfNkoma, wakati wa kufanya tafiti za namna gani wataweza kupunguza bei hizo, pia waliangalia na nchi nyingine wanavyofanya ambapo nyingi zimeonekana zimeanza siku nyingi kutoza kiasi kidogo katika mwingiliano huo wa mitandao.
Aliongeza kuwa, walitumia kampuni moja ya Uingereza katika kufanya tafiti hiyo, ambapo mbali na mambo mengine waliangalia gharama za uendeshaji ambazo makampuni ya simu hapa nchini yamekuwa yakitumia, hivyo wana uhakika hakuna atakayepata hasara kutokana na mabadiliko hayo.
Akifafanua zaidi kuhusu bei hizo elekezi, alisema zitakuwa zinashuka mwaka hadi mwaka ambapo hadi kufika mwaka 2017 mteja atakuwa akitozwa sh 26.96 kwa dakika.
Lengo la kufanya hivyo, mkurugenzi huyo alisema ni katika kuona kila mwananchi ana uwezo wa kupata huduma hiyo ya mawasiliano ambayo inakuwa siku hadi siku.
0 comments:
Post a Comment