BAADA ya kufanyika jijini Dar es Salaam maonesho makubwa ya mavazi ya Kiswahili ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ‘Swahili Fashion Week’, sasa yanatarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar kwenye ukumbi wa Mbweni Ruins, Februari 15, mwaka huu.
Akizungumza jana, muandaaji wa Swahili Fashion Week, Mustafa Hassanali, alisema kwamba, wameamua kupeleka onesho hilo visiwani humo ili kutoa nafasi kwa wadau wa huko nao kuyashuhudia.
“Sisi tunawajali sana wadau wetu, ndiyo maana SFW tumekuwa tukiipeleka sehemu mbalimbali mbali na lile onesho kubwa kabisa linalofanyika jijini Dar es Salaam kila mwaka,” alisema Hassanali.
Hassanali ambaye pia ni mbunifu maarufu wa mavazi, aliongeza kuwa, katika onesho hilo wabunifu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kuonesha kazi zao.
Awali, SFW ilifanyika Desemba 6 hadi 8 mwaka jana, katika Hoteli ya Golden Tulip, ikiwa ni mara ya tano tangu kuanzishwa kwake, ambapo wabunifu wa mitindo zaidi ya 50 kutoka nchi mbalimbali duniani walionesha kazi zao.
Mbali na maonesha ya mavazi, SFW pia ilihusisha ‘Shopping Festival’, shindano la wabunifu wa mitindo chipukizi, warsha ya wabunifu, kumtafuta mbunifu bora anayechipukia, mbunifu bora wa kubuni fulana, pamoja na utoaji tuzo kwa wadau waliokuwa mstari wa mbele katika masuala ya mitindo.
0 comments:
Post a Comment