WASANII Peter Msechu wa Tanzania na Cheikh Lo kutoka Senegal wanatarajiwa kushambulia jukwaa pamoja na wanamuziki wengine zaidi ya 100, kwenye tamasha la Sauti za Busara 2013 ndani ya viunga vya Ngome Kongwe, Zanzibar.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Sauti za Busara, Simai Saidi, alisema tamasha hilo la 10, limepangwa kufanyika kuanzia Februari 14 hadi 17, visiwani humo sambamba na kutolewa warsha mbalimbali kwa wasanii na wadau.
Simai alisema kuwa kwa sasa Sauti za Busara imefikia kiwango cha juu na kuwa hadhi ya Afrika Mashariki na kielelezo tosha katika kutangaza utalii wa ndani na kuongeza uchumi mbali ya burudani.
“Tunashukuru wadau kwa muda wa miaka 10 hadi kufikia hapa, tunaendelea kuwaomba kusaidia tamasha hili ili lizidi kupasua anga za kimataifa,” alisema Simai.
Aliongeza kuwa tamasha hilo limesaidia kuongeza mapato katika utalii na kutoa ajira kwa watu mbalimbali.
Aidha wasanii nyota Peter Msechu wa Tanzania na Cheikh Lo wa Senegal watakuwa kivutio kwenye tamasha hilo, ambalo pia hukusanya wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Wasanii wengine ni pamoja na bendi ya DDC Mliman Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’, Culture Musical Club Zanzibar, Khaira Arby Mali, Comrade Fatso na Chabvondoka Zimbabwe, Atongo Zimba Ghana, N’Faly Kouyaté Guinea, Nathalie Natiembe Reunion, Nawal & Les Femmes de la Lune na Comoro/Mayotte.
Wengine na nchi zao kwenye mabano ni Wazimbo (Msumbiji), The Moreira Project (Msumbiji/Afrika Kusini), Owiny Sigoma Band (Kenya/Uingereza), Mokoomba (Zimbabwe), Msafiri Zawose &; Sauti Band (Tanzania), Mani Martin (Rwanda), Burkina Electric (Burkina Faso/Marekani), Lumumba Theatre Group (Tanzania), Sousou & Maher Cissoko (Senegal/Sweden), Super Maya Baikoko (Tanzania).
Aidha tamasha hilo litakuwa na mtandao maalumu (Movers & Shakers) kwa wenyeji na wageni wataalamu katika sanaa na kujadili maendeleo ya muziki Afrika, pamoja na shughuli za Busara Xtra ambazo zitafanyika nje ya ukumbi huo wa Ngome Kongwe.
Tamasha hilo limedhaminiwa na Goethe Institute, Grand Malt, Memories of Zanzibar, Diamond Trust Bank, ChemiCotex, Azam Marine, Ultimate Security, Zanzibar Unique Ltd, Southern Sun, Embassy of France, Alliance Française, Smole II na wengine wengi.
0 comments:
Post a Comment