BENKI Kuu ya Tanzania
(BoT) imeruhusu kuwapo shughuli za uwakala utakaotoa fursa kwa mtu au kampuni
kuingia mkataba na benki yoyote nchini na kuendesha huduma kama wakala kwa
niaba ya benki husika.
Lengo la kuanzisha huduma
za uwakala wa benki nchini ni kuwezesha wananchi kupata huduma za kifedha kwa
karibu na kirahisi zaidi pamoja na kuweka mfumo sawa wa utoaji huduma hizo
katika njia ambayo inatoa unafuu wa gharama kwa watumiaji.
Mkurugenzi wa Huduma za
Kibenki wa BoT, Emmanuel Boaz alisema jana kuwa kupitia wakala, benki zitatumia
maduka, vituo vya mafuta, shule na taasisi kadhaa kutoa huduma bila kulazimika
kujenga majengo ya matawi.
Alisema benki
zitaruhusiwa kutoa huduma kupitia wakala baada ya kupata kibali kutoka BoT na
kwamba utoaji wa kibali utazingatia utimizaji vigezo vilivyoainishwa katika
mwongozo ikiwa ni pamoja na kuwa na mtaji.
Alitaja vigezo vingine kuwa ni kuthibitisha
uwezo kimapato na kuwa na historia nzuri ya kutimiza matakwa ya kisheria,
kanuni na maelekezo kuhusu biashara ya benki.
Boaz alisema benki
zitakazoruhusiwa kufanya hivyo zitatakiwa kuwa na mkataba unaozingatia mwongozo
wa uwakala. Alisema mkataba hautakuwa na kipengele cha kuzuia wakala kuingia
mkataba wa uwakala na benki zingine.
Alitaja baadhi ya vigezo
vya uwakala kuwa ni mhusika awe amefanya biashara halali kisheria katika muda
usiopungua miaka miwili na biashara husika iwe endelevu.
Alisisitiza kuwa biashara
ya wakala wa benki haitafanywa na kampuni au mtu yeyote asiye na biashara
nyingine ya msingi.
Alisema vigezo vingine ni
pamoja na kuwa na leseni ya biashara, kuwa na sehemu ya kudumu ya biashara,
kutokuwa na mkopo chefuchefu katika benki; kuwa na wafanyakazi wenye uwezo wa
kufanya uwakala.
Alisema wakala atakuwa
akipokea na kutoa amana za wateja, kusaidia wateja wenye amana kufanya malipo
na ulipaji mikopo. Shughuli zingine ni kusaidia wateja kulipa Ankara na kufanya
malipo kwa ajili ya akiba ya uzeeni.
Mawakala pia watasaidia
wateja wa benki kutuma fedha ndani na nje ya nchi, maulizo ya salio na kutoa
kwa wateja wa benki ripoti fupi ya akaunti zao.
0 comments:
Post a Comment