Saturday, November 23, 2013

leo kama zamani

Jumapili, Novemba 24, 2013Leo ni Jumapili tarehe 20 Muharram mwaka 1435 Hijria, sawa na tarehe 24 Novemba 2013 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 381 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa masuala ya jamii wa Uholanzi Baruch de Spinoza. Baada ya Spinoza kuhitimu elimu ya juu, alivutiwa sana na elimu ya falsafa ya Descartes. Ukosoaji mkubwa wa mwanafalsafa huyo dhidi ya itikadi za dini ya Kiyahudi ulizusha uhasama mkubwa wa viongozi wa dini hiyo na kuanzisha kampeni za kumtenga katika jamii yao. Fikra za kifalsafa za Spinoza zinakaribiana sana na itikadi za kisufi.
Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni 'Sayansi ya Maadili', 'Siasa' na 'Marekebisho ya Akili'.
Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita lilianza kuchapishwa gazeti la Majlis nchini Iran. Gazeti hilo lilikuwa na kurasa 8. Mbali na kuandika habari za ndani na nje, gazeti hilo lilikuwa likiakisi pia mazungumzo ya vikao vya Bunge la Taifa la Iran. Mhariri Mkuu wa gazerti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo.
Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa Henri Toulouse Lautrec wa Ufaransa. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na pamoja na kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Henri Toulouse alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901 Miladia.
Na siku kama ya leo miaka 182 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza alifanikiwa kugundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa jina la ''Electric Current''. Ugunduzi huo ulimuwezesha Faraday kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbali vya kielimu na kuweza kufikia kipawa kikubwa cha elimu sanjari na kugundua vyombo vingi vya umeme katika uwanja huo. na Sudi Jafar Shaban

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...