Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco), limeomba kuongeza bei ya umeme kwa asilimia
67.87 ikiwa ni kutoka Sh197.8 kwa Unit mpaka Sh332.06.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alipokuwa akiwasilisha maombi
ya shirika hilo mbele ya Wadau wa Umeme na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura).
Alisema kwa sasa uzalishaji wa umeme
utokanao na nguvu za maji ni asilimia 13, utokanao na gesi ni asilimia
42 na utokanao na mitambo ya mafuta ni asilimia 45.
"Kutokana na kuongezeka kwa gharama za
kutoa huduma, wastani wa bei iliyopo ya Sh197.8 kwa uniti, hailingani
na wastani wa Sh332.06 kwa unit inayotakiwa kukidhi mahitaji ya sasa,"
alisema Mramba na kuongeza:
"Hii ni pungufu kwa kiasi cha Sh134.25 kwa uniti, ongezeko la bei la asilimia 67.87 litafidia upungufu huo," alisema Mramba.(P.T)
Alisema madhara mengine yatokanayo na kutoongezwa kwa bei hiyo ni shirika hilo kutokidhi mikataba iliyoingiwa jambo alilosema litasababisha mgogoro ya kimikataba.
Mramba alieleza pia kuwa, hali hiyo italifanya shirika hilo kushindwa kulipa mikopo yake benki na kuathiri uwezo wake wa kuwekeza kupitia mikopo mipya.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013 matumizi ya umeme yamekuwa yakiongezeka wakati kiwango cha mvua kikiwa chini ya wastani hali iliyosababisha Tanesco kutumia zaidi umeme unaozalishwa kwa mafuta.
"Katika kipindi hiki kiwango cha gesi asili hakikukidhi mahitaji ya nishati kwa sababu ya ufinyu wa miundombinu ya gesi iliyopo. Upungufu huu ulisababisha mgawo wa umeme mwaka 2010 na 2011," alisema na kuongeza:
Katika hatua nyingine, Mramba alisema kutokana na gharama za uzalishaji kupanda, hasara ndani ya shirika hilo imeongezeka kutoka Sh43.43 bilioni mwaka 2011 hadi Sh178.45 bilioni mwaka 2012.
Kwa upande wake, Shirikisho la Watu Wenye Viwanda (CTI), lilipinga viwango hivyo likisema kuwa sababu zilizotolewa na Tanesco hazina mashiko.
"Lazima kuwe na sababu zinazoeleweka, lakini Tanesco sababu ilizoleta siyo za msingi, lazima kwanza waangalie uendeshaji wao, kukusanya madeni na kudhibiti upotevu wa umeme," alisema mwakilishi wa CTI, Dk Samuel Nyangahe.
Alieleza kuwa, Tanesco kutaka kupandisha bei ya umeme bila kudhibiti mapato yake na uendeshaji wa shirika hilo, kamwe hakuwezi kuwa suluhu ya hasara ambayo shirika hilo linasema linaipata.
"Kwanza wakiongeza bei na watu watapunguza matumizi kwa hiyo haitawasaidia," alisema.
Januari mwaka 2012, Ewura iliidhinisha nyongeza ya bei ya dharura kwa wastani wa asilimia 40.29, ombi la Tanesco lilikuwa ni kutaka bei hiyo iongezwe kwa asilimia 155.
via......... mjegwa blog
0 comments:
Post a Comment