
Mlinda mlango kutoka nchini Poland, Lukasz Fabianski ameonyesha kukunwa na mafanikio ya kutwaa ubingwa wa kombe la FA kwa Arsenal huku akitarajia kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa mwezi huu.
Lukasz Fabianski, ambae alikuwa shujaa katika michezo yote ya kombe la FA msimu huu ameonyesha hisia hizo tangu akiwa kwenye mchezo wa hatua ya fainali, ambapo Arsenal walimaliza kwa nderemo na vifijo baada ya kupata ushindi wa mabao matatu kwa mawili.
Fabianski, amesema imekua faraja kubwa sana kwake kumaliza jukumu la kuitumikia klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London, kwa kutwaa taji muhimu, hali ambayo anaamini imemtofautisha na wachezaji wengine walioondoka kwenye klabu hiyo wakiwa mikono mitupu.
Amesema kutokana na kazi ya mikono yake, hana budi kujipa pongezi na kuanza kufikiria maisha yake baada ya kuondoka Arsenal mwishoni mwa mwezi huu, ambapo mkataba wake utakua unafikia kikomo.
“Sina namna ya kujizuia kwa furaha isiyo na kifani, ninalazimika kusema chochote kwa kuonyesha hisia za furaha niliyo nayo, ni bahati iliyoje kwangu kufikia mafanikio makubwa kama haya.” Amesema Fabianski.
“Ilikuwa kama ndoto kwangu ambayo haikutimizwa kwa kipindi chote nilichokuwepo hapa tangu mwaka 2007, lakini nimejaaliwa kuipata zawadi ya kombe la FA msimu ambao nimedhamiria kuipa mkono wa kwaheri klabu ya Arsenal ambayo bado ninaipenda.”
Lukasz Fabianski mwenye umri wa miaka 29, alisajiliwa na klabu ya Arsenal mwaka 2007 akitokea nchini kwao Poland alipokuwa akiitumikia klabu ya Legia Warsaw.
Mchezo wa hatua ya fainali ya kombe la FA ulikuwa ni mchezo wa 78 kwa mlanda mlango huyo, ambae anaondoka Emirates Stadium, kutokana na mkataba wake kufikia kikomo, huku akishinikiza kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza ambayo kwa sasa inashikiliwa na Wojciech Szczesny.
Fabianksi, anaungana na beki wa pembeni kutoka nchini Ufaransa Bacary Sagna kuondoka klabuni hapo, kufuatia beki huyo mwenye umri wa miaka 31, kugoma kusaini mkataba mpya.
Wakati huo huo kikosi cha Arsenal pamoja na meneja Arsene Wenger, jana walitumia muda mwingi kulitembeza kombe la FA katika mitaa ya kaskazini mwa jiji la London kwa lengo la kuendeleza sherehe za kutwaa ubingwa huo sambamba na mashabiki wao.
Angalia video ya wachezaji wa Arsenal pamoja na meneja Arsene Wenger walivyokuwa wakipita mitaani wakiwa na mwali wa FA.
No comments:
Post a Comment