
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kufanya upya sensa ya
mifugo kwani ya mwisho ilifanyika miaka 30 iliyopita.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana (Ijumaa, Septemba 5, 2014) wakati akifungua mkutano wa
siku tatu wa wadau wa mifugo hapa nchini ulioanza leo kwenye hoteli ya
Malaika jijini Mwanza.
Waziri Mkuu
amesema ni vigumu kwa wafugaji kutaja idadi halisi ya mifugo waliyonayo
lakini kama Wizara hawana budi kuweka mbinu za kisasa za kufanya sensa
hiyo hata kama itawachukua miaka miwili.
“Hizi takwimu
kwamba Tanzania ina idadi ya ng’ombe milioni 22.8 zinaweza zisiwe sahihi
sana. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 1984… Hizi takwimu zitakuwa ni
za kutoka kwa watendaji tu hapa na pale. Na mara nyingi ukiwauliza
wafugaji wanakutajia idadi ndogo wakati idadi halisi wanaificha.
Tunahitaji kufanya sensa halisi ya mifugo hapa nchini,” alisema.
Aliwaeleza
washiriki wa Mkutano huo kwamba mifugo ni sekta muhimu hasa ikizingatiwa
kwamba inawawezesha wananchi kupata milo yao. “Ukichukua kilimo, hakuna
mtu ambaye hana kijishamba japo kidogo. Kwenye mifugo hakuna anayekosa
walau kuku au bata wa kufuga, kwenye uvuvi nako watu wanaenda baharini
au ziwani kila kukicha ili kupata chochote na kwenye misitu nako kuna
rasilmali zinazotokana na misitu na kubwa ni zao la asali,” alisema huku
akishangiliwa.
Alisema fursa
zilizopo hazitumiki ipasavyo kwa sababu watendaji wengi wamezoea kukaa
ofisini badala ya kwenda waliko wananchi na kuwaelimisha jinsi
wanavyoweza kunufaika na fursa hizo. “Fursa zipo nyingi, kikubwa ni
kujipanga vizuri na kumwezesha Mtanzania wa kawaida atumie fursa hizo
ili kubadilisha maisha yake,” alisema.
“Tunatakiwa
kumbadilisha fikra mfugaji mdogo ili aone ng’ombe alionao ni fursa.
Tubadili fikra za mfugaji huyu mdogo ili aone umuhimu wa kufuga ng’ombe
wachache watakaolishwa vizuri na kumpatia kipato kikubwa. Aone kuna tija
katika idadi ndogo ya mifugo badala ya kufurahia uwingi wao,”
aliongeza.
Alisisitiza haja
ya wataalamu kuwafundisha wafugaji aina nyingine za ufugaji badala ya
kung’ang’ania ngombe tu na mbuzi. “Hivi sasa kondoo wana soko kubwa sana
Uarabuni kwa sababu wanasema nyama yake haina cholesterol (lehemu).
“Kuna kuku wa
chotara sasa hivi wanauzwa kuanzia sh.35,000/-. Mtu akiwa na kuku 100
hii ni fursa nzuri tu. Nilitembelea banda la Ukerewe kwenye maonyesho ya
NaneNane hapa Mwanza, nikakuta mtu anafuga bata mzinga, kuuliza bei
gani akajibu mmoja anauzwa sh. 180,000/-. Kama ni Dar es Salaam huyo
bata mzinga angeuzwa kwa sh.4000,000/-. Tutumie fursa hizi, tuwaelimishe
wananchi wetu ili waweze kutoka hapo walipo,” alisema.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani alisema licha ya kuwepo idadi kubwa ya
mifugo nchini, Watanzania bado hawajaweza kufikia kiwango kinachotakiwa
cha ulaji wa bidhaa za mifugo kama mayai, nyama na maziwa.
“Mtanzania kwa
wastani anakula mayai 72 kwa mwaka, lita za maziwa 45 na kilo 11 za
nyama kwa mwaka wakati kiwango kinachotakiwa ni mayai 300, lita 200 za
maziwa na kilo 50 za nyama kwa mwaka. Bado tuna kazi kubwa ya
kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kula bidhaa zinazotokana na
mifugo,” alisema.
Alisema sekta
hiyo haijapata uwekezaji mkubwa katika ufugaji na usindikaji wa mazao ya
mifugo na kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo tatizo la
uhaba wa nyanda za malisho, ambalo limesababisha wafugaji kuhamahama,
ukosefu wa maji hasa wakati wa kiangazi, magonjwa ya mifugo na uhaba wa
watumishi katika ngazi ya Halmashauri.
Mkutano huo wa
Kitaifa unahudhuriwa na Mawaziri kutoka Wizara mtambuka za Ardhi na
Maendeleo ya Makazi; Kilimo, Chakula na Ushirika na Ofisi ya Waziri Mkuu
(TAMISEMI); Wakuu wa Mikoa 14 ya Geita, Njombe, Tanga, Morogoro, Rukwa,
Katavi na Kagera. Mingine ni Dodoma, Tabora, Manyara, Pwani,
Kilimanjaro, Iringa na Mbeya. Washiriki wengine ni Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri, wadau wa sekta hiyo ambao ni
wakulima na wafugaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment