Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza leo kuwa dawa za chanjo ya
Ebola huenda zikaanza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu katika kipindi
cha wiki mbili zijazo.
Akitoa tangazo hilo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva,
Mkurugenzi Msaidizi wa WHO kuhusu habari na mifumo ya afya, Dr. Marie
Paule Kieny, amesema kuna aina mbili za chanjo dhidi ya Ebola, ambazo
majaribio yake yataanza wiki mbili zijazo:
"Majaribio haya yataendelea kwa miezi sita hadi mwaka mmoja,
lakini kuwa na matokeo ya awali kuhusu usalama wake na kufanya uamuzi
kuhusu dozi yake, itakuwa mwishoni mwa mwaka huu, Disemba."
Majaribio ya chanjo hiyo yatahusisha watu 250 watakaojitolea, wakiwa
kati ya umri wa miaka 18 na 65, na wenye afya nzuri. Dr. Kieny ameelezea
umuhimu wa majaribio haya
"Majaribio haya yatashirikisha idadi kubwa zaidi ya watu
wanaojitolea, na yatakuwa muhimu sana katika kuamua usalama na kinga
dhidi ya Ebola, na takwimu hizo zitakuwa muhimu mno katika kufanya
uamuzi kuhusu kipimo cha dozi kitakachotumiwa katika kupima ubora wa
chanjo hiyo Afrika"
Majaribio yakihitimishwa, chanjo ya Ebola inatarajiwa kuanza kutumiwa
Afrika Magharibi mapema mwakani. Haijulikani ni lini chanjo itaanza
kutolewa kwa umma kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment