Imeandikwa na Malisa Godlisten
Ninaandika makala hii nikitambua bayana kuwa itamuudhi kila mtu
anayeingia mtandaoni kwa minajili ya kuwanyanyasa wengine. Lakini siku
zote ninaamini katika busara hii: kuuchukia ukweli hakubadilishi ukweli
kuwa uongo. Ukweli ni ukweli na uongo ni uongo. Ukweli hauwezi kuwa
uongo, na kadhalika uongo hauwezi kuwa ukweli. Kamwe asilani. Wakati
tunaomboleza kifo cha ndugu yetu Betty Ndejembi watu wamesema mengi, na
yameandikwa mengi. Kila mmoja kwa namna alivyoguswa. Zitto kabwe
ametweet hivi asubuhi “justice for bett”, akitoa rai haki ipatikane
kwenye kifo cha Betty.
Marehemu Betty Ndejembi
Jokate Mwegelo naye ametweet kuomba msaada wa kuchunguza kifo cha
Betty. Na watu wengine maarufu kila mmoja kasema neno, labda kwa sababu
Betty alikuwa maarufu in one way or another. Lakini hatuwezi kukwepa
ukweli kwamba siku chache kabla ya kifo chake, alinyanyaswa mno kwenye
mtandao wa kijamii wa Twitter.
Japo hadi muda huu hatuwezi kuhusisha moja kwa moja uhusiano kati ya
unyanyasaji huo na kifo chake, lakini mtu akinyanyaswa masaa kadhaa
kabla ya kifo chake, waweza kujenga picha fulani. Saa chache kabla ya
kifo chake Betty alitweet, “ITS ALWAYS THE PEOPLE YOU TRUST WILL DO
THEOST DAMAGE TO YOU...ITS BEEN A GOOD LIFE THO”
Baada ya kutweet hakuonekana tena hadi alipookotwa mtaroni kesho yake
asubuhi akiwa amefanyia vitendo vya kikatili na akiwa amepoteza fahamu.
Lakini kabla hata ya kutweet hivyo, Betty alikuwa anaandamwa sana
mtandaoni huko Twitter. Kuna watu walianzisha team ya kumtukana, kumjibu
hovyo na kumprovoke kwa kila alilofanya. Naomba ieleweke kuwa simlaumu
mtu kwa sababu sina mamlaka ya kufanya hivyo bali dhima ya makala hii ni
rambirambi zangu kwa Betty kuzungumzia tatizo la unyanyasaji mtandaoni,
sambamba na suala zima la unafiki kila kinapojiri kifo hususani cha mtu
maarufu. Tuna tatizo kubwa huko mitandaoni.
Tumefika hatua ya kuwapa umaarufu watu wenye matusi ya nguoni,
wazushi, wambeya, wanafiki. Wanaochafua wenzao, kutishia wenzao kwa
kujifanya askari jkt, kusengenya na kupost majungu…. Aina ya binaadamu
wanaostahili laana lakini twaishia kuwatukuza
Kwenye hii mitandao, matusi imekuwa njia ya mkato ya kupata umaarufu.
Kuna wenzetu wengi tu wenye ‘umaarufu’ huko twitter, facebook na
instagram lakini ukidadisi chanzo cha ‘umaarufu’ huo, utaambiwa ‘ah huyu
ana matusi si mchezo’. Kuna watu wazima na akili zao wanatumia muda
mwingi kwenye mitandao ya kijamii aidha kunyanyasa wenzao kama si
kusherehesha unyanyasaji huo. Marehemu Betty ni victim wa yote hayo.
Alitukanwa sana, na aliitwa majina kadhaa ya kumdhihaki kabla ya kukutana na mauti.
Kuna waliomwita Di maria, superstar uchwara etc.. and I hope hao
waliomuita hivyo wanajifahamu na wengine wananisoma hapa. Japo sijui
chanzo cha ‘ugomvi’ wao, lakini naamini kuna watu wengi tu waliokuwa
katika nafasi ya kuzima moto huo kwa vile walikuwa wakizifahamu pande
zote mbili za ‘ugomvi’ husika lakini kwa sababu ya unafiki wakapalilia
moto maana wanafurahi watu wakigombana.
La kukera zaidi ambalo ni wazi litajichomoza wakati wa maombolezo
haya ni unafiki. Watu walewale waliodiriki kumwandama marehemu wakati wa
uhai wake watageuka kuwa wenye uchungu mkubwa baada ya kifo chake.
Hii inanikumbusha suala ambalo nimeshawahi kulizungumzia mara kadhaa
kwamba ‘wakati’ muafaka wa kutafuta vipaji vya uigizaji ni kwenye
misiba: watu walewale waliokuwa wakikuchukia kwa nguvu zote watageuka
wenye uchungu mkubwa kwa kifo chako.’ Ukiangalia baadhi ya tweets za
mwisho za marehemu ni wazi kuwa binti huyo alikuwa anahitaji msaada
kutoka kwa wanaomjali. Mojawapo ya tweet za mwishomwisho za marehemu
alisema hivi.
‘Thank you all for the names I was called, luck y’all have such a
perfect life.! No hard feelings.. I’m alive still.! Endeleeni kuongea.’
Kwa tafsiri isiyo rasmi Betty alisema, ‘asanteni kwa majina yote
mliyoniita. Mmebarikiwa kuwa na maisha mazuri.! Hamuumizwi na hisia kama
mimi. Ila bado ninaishi, endeleeni kuongea.’
Kwa bahati mbaya hakuna aliyejali, hadi juzi asubuhi (Jumatano) Betty
alipookotwa kwenye mtaro akiwa amefanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na
akiwa amepoteza fahamu. Kifo cha Betty ni miongoni mwa vifo vya kikatili
sana kuwahi kutokea nchini. Nashauri wanaharakati ea haki za wanawake
wapambane kuhakikisha haki inapatikana.
Akina Annanilea Nkya, Hellen Kijobisimba watafute haki ya binti huyu
kama Zitto Kabwe alivyosema ‘justice for betty’, imagine mtu aliyekua
kwenye maumivu makali ya hisia, anatekwa na genge la wahuni. Bila kujali
kipindi kigumu alichokua anapitia, bila kujali hakua na wazazi, bila
kujali psychological torture aliyokua nayo still wanamfanyia unyanyasaji
wa kijinsia hadi anapoteza fahamu.
Betty aliokotwa mtaroni na kupelekwa hospitali. Jana (Alhamisi)
aliweza kufungua macho, lakini hakuweza kuongea lolote hadi saa 3 usiku
wa kuamkia leo, mauti ilipomkuta. Kwaheri betty, kwaheri classmate wangu
(Majengo sec). Kwaheri rafiki, kwaheri ndugu. Umeondoka dunia bado
inakuhitaji. Naumia you have gone too young, lakini naumia zaidi sababu
umekufa kikatili mno.
Japo sijui nitakufaje, lakini nadiriki kusema hukustahili kifo cha
aina hii. Nakumbuka sms yako ya mwisho kwangu uliniambia hivi, ‘Malisa
blv me, only youths can change this country.’ Leo nilipopata taarifa ya
kifo chako nimerudia kuisoma sms yako mara mbilimbili.
Sikujua kuwa sms hiyo ndo ulikua unaniaga. Umeniaga kwa kutuachia
vijana wosia, kuwa vijana pekee ndio wenye uwezo wa kuibadilisha nchi
hii. Nitakua nimekusaliti ikiwa sitautendea kazi wosia huu. I promise to
fight and motivate other youths to liberate this country for your
dedication. Umekwenda kumfuata mama yako, umemfuata baba yako. Wazazi
wako walitangulia, leo wewe umewafuata. Hatimaye familia nzima mmekutana
Paradiso.
Huu ni baadhi ya ujumbe uliondikwa na watu mbalimbali waliokuwa wakimfahamu Betty:
Faraja Nyalandu:
Kifo cha Betty kimetuachia mafundisho mengi. Natumai kila mmoja
aliyemfahamu Betty kwa namna moja ama nyingine amepata lake la
kujifunza. Gharama ya mafundisho tuliyoyapata ni kubwa sana. Maumivu.
Kifo. Aliyelipa ni Betty na wanaompenda. Itafaa gharama hii isiende
bure. Tuwe wakarimu. Tuwe na upendo. Tumshike mtu mkono pale alipo na
uhitaji. Tumnyanyue akianguka. Lakini vyote haviwezi kuwa kama ndani
yetu havipo. Huwezi kutoa ambacho huna. Tuanze ndani yetu. Betty
tusamehe. Mungu atusamehe na Mungu atusaidie. Pumzika kwa amani Betty.
Ukatili na unyanyasaji wa aina yoyote ni kinyume cha haki za
binadamu, tupaze sauti kwa pamoja na kuchukua hatua. Vitendo hivi
havikubaliki.
‘Justice for Betty’..Apumzike kwa Amani.